5:17 PM
5. Mtu anawezaje kuanzisha uhusiano wa kawaida na Mungu?

Maneno Husika ya Mungu:

Watu wanaamini katika Mungu, wanampenda Mungu, na kumkidhi Mungu kwa kugusa Roho wa Mungu kwa moyo wao, hivyo kupata ridhaa ya Mungu; na wakati wanajihusisha na maneno ya Mungu kwa moyo wao, kwa hivyo wanasisimuliwa na Roho wa Mungu. Ikiwa unataka kufikia maisha ya kawaida ya kiroho na kuanzisha uhusiano wa kawaida na Mungu, lazima kwanza uutoe moyo wako kwa Mungu, na uuweke moyo wako uwe mtulivu mbele za Mungu. Baada tu ya kuutoa moyo wako mzima katika Mungu ndipo utaweza kuwa na maisha ya kawaida ya kiroho hatua kwa hatua. Kama, kwa imani yao katika Mungu, watu hawautoi moyo wao kwa Mungu, ikiwa moyo wao hauko katika Mungu, na wala hawauchukulii mzigo wa Mungu kama wao wenyewe, basi kila kitu wanachofanya ni kumdanganya Mungu, nayo ni matendo ya watu wa kidini, wasioweza kuipokea sifa ya Mungu.

kutoka katika “Ni Muhimu Sana Kuanzisha Uhusiano wa Kufaa na Mungu”katika 

Neno Laonekana katika Mwili

Maneno halisi ya Roho Mtakatifu ni nguvu za kazi ya Roho Mtakatifu, na kuendelea kwa Roho Mtakatifu kumpa nuru mwanadamu wakati wa kipindi hiki ni mwelekeo wa kazi ya Roho Mtakatifu. Na mwelekeo ni upi katika kazi ya Roho Mtakatifu leo? Ni uongozi wa watu ndani ya kazi halisi ya Mungu, na ndani ya maisha ya kiroho ya kawaida. …

Kwanza, lazima uumimine moyo wako ndani ya maneno ya Mungu. Lazima usiyafuatilie maneno ya Mungu katika siku za zamani, na lazima usiyasome wala kuyafananisha na maneno ya sasa. Badala yake, lazima uumimine moyo wako kabisa katika maneno halisi ya Mungu. Kama kuna watu ambao bado wangependa kuyasoma maneno ya Mungu, vitabu vya kiroho, au maelezo mengine ya mahubiri kutoka kwa siku za zamani, ambao hawafuati maneno halisi ya Roho Mtakatifu, basi wao ni wapumbavu zaidi ya watu wote; Mungu huchukia sana watu kama hao. Kama uko radhi kukubali nuru ya Roho Mtakatifu leo, basi mimina moyo wako kabisa katika matamshi halisi ya Mungu. Hili ni jambo la kwanza ambalo lazima utimize.

kutoka katika “Jua Kazi Mpya Zaidi ya Mungu na Fuata Nyayo za Mungu” katika

Neno Laonekana katika Mwili

Ni kwa kuja kumjua Mungu tu na kumridhisha kwa msingi wa kula na kunywa maneno Yake ndipo mtu anaweza kuanzisha polepole uhusiano unaofaa na Yeye. Kula na kunywa maneno Yake na kuyaweka katika matendo ni ushirikiano bora zaidi na Mungu, na ni kitendo kinachotoa ushuhuda vizuri zaidi kama mmoja wa watu Wake. … Ili kutimiza maisha ya kiroho ya kufaa, kwanza kula na kunywa maneno ya Mungu na kuyaweka katika vitendo; na juu ya msingi huu anzisha uhusiano wa kufaa kati ya mwanadamu na Mungu.

kutoka katika “Wale Ambao Tabia Yao Imebadilika ni Wale Ambao Wameingia

Katika Uhalisi wa Neno la Mungu” katika Neno Laonekana katika Mwili

Katika kuwa na imani kwa Mungu, ni lazima angalau utatue swala la kuwa na uhusiano wa kawaida na Mungu. Bila uhusiano wa kawaida na Mungu, basi umuhimu wa kumwamini Mungu unapotea. Kuunda uhusiano wa kawaida na Mungu kunapatikana kikamilifu kupitia kuutuliza moyo wako mbele ya Mungu. Uhusiano wa kawaida na Mungu unamaanisha kuweza kutoshuku au kukataa kazi yoyote ya Mungu na kutii, na zaidi ya hayo unamaanisha kuwa na nia sahihi mbele ya Mungu, sio kufikiria kujihusu, daima kuwa na maslahi ya familia ya Mungu kama jambo muhimu zaidi haijalishi kile unachofanya, kukubali kutazamiwa na Mungu, na kukubali mipangilio ya Mungu. Una uwezo wa kuutuliza moyo wako mbele ya Mungu kila unapofanya chochote; hata kama huelewi mapenzi ya Mungu, bado ni lazima utimize wajibu na majukumu yako kadri ya uwezo wako. Hujachelewa sana kusubiri mapenzi ya Mungu yafichuliwe kwako na kisha kuyaweka katika vitendo. Wakati uhusiano wako na Mungu umekuwa wa kawaida, basi pia utakuwa na uhusiano wa kawaida na watu. Kila kitu kimejengwa juu ya msingi wa maneno ya Mungu. Kupitia katika kula na kunywa maneno ya Mungu, tenda kulingana na mahitaji ya Mungu, weka sawa maoni yako, usitende mambo yanayompinga Mungu au kuingilia kati mambo ya kanisa. Usifanye vitu visivyo na manufaa kwa maisha ya ndugu, usiseme maneno yasiyosaidia wengine, usifanye vitu vya kufedhehesha. Kuwa mwadilifu na mwenye heshima unapofanya mambo yote na kuyafanya ya kupendeza mbele ya Mungu. Hata ingawa kutakuwa na nyakati ambazo mwili ni dhaifu, unaweza kushikiza umuhimu mkubwa kabisa kwa kufaidi familia ya Mungu, kutotamani faida yako mwenyewe, na kutekeleza haki. Ikiwa unaweza kutenda kwa njia hii, uhusiano wako na Mungu utakuwa wa kawaida.

Kila unapofanya chochote, lazima uchunguze iwapo motisha yako ni sahihi. Ikiwa unaweza kutenda kulingana na matakwa ya Mungu, basi uhusiano wako na Mungu utakuwa wa kawaida. Hiki ndicho kigezo cha chini zaidi. Iwapo, unapochunguza motisha yako, kunatokea zile zisizo sahihi, na iwapo unaweza kuzikwepa na kutenda kulingana na maneno ya Mungu, basi utakuwa mtu ambaye ni mwema mbele ya Mungu, kitu ambacho kitaonyesha kuwa uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida, na kwamba kila unachofanya ni kwa ajili ya Mungu, na sio kwa sababu yako binafsi. Ni lazima uuweke moyo wako sawa kila unapofanya ama kusema chochote, uwe mwenye haki katika matendo yako, na usiongozwe na hisia zako, au utende kulingana na mapenzi yako: Haya ndiyo maadili ambayo wale wanaoamini katika Mungu wanatenda kulingana nayo. Motisha za mtu na kimo chake vinaweza kufichuliwa katika kitu kidogo, na hivyo, kwa watu kuingia kwa njia ya kufanywa wakamilifu na Mungu, ni lazima kwanza wasuluhishe motisha yao wenyewe na uhusiano wao na Mungu. Ni pale ambapo tu uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida ndipo utaweza kufanywa mkamilifu na Mungu, na ni hapo tu ndipo ushughulikiaji, upogoaji, nidhamu, na usafishaji wa Mungu kwako utaweza kupata matokeo yanayotakiwa. Hiyo kusema, watu wanaweza kuwa na Mungu mioyoni mwao, wasitafute maslahi binafsi, wasifikirie kuhusu maisha yao binafsi ya baadaye (ikirejelea kufikiri juu ya mwili), lakini badala yake wanabeba mzigo wa kuingia katika maisha, wanajitahidi wawezavyo kutafuta ukweli, na kuitii kazi ya Mungu. Kwa namna hii, makusudi unayoyatafuta ni sahihi, na uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida.

kutoka katika “Uhusiano Wako Na Mungu Ukoje” katika Neno Laonekana

katika Mwili

Madondoo ya Mahubiri na Ushirika kwa ajili ya Marejeo:

Tunapoanzisha uhusiano wa kufaa na Mungu, tunapaswa kuanzia wapi? Jambo muhimu zaidi ni kuzungumza kutoka moyoni wakati wa kuomba kwa Mungu. Kwa mfano, unasema katika sala, “Ee Mungu, naona kwamba ndugu zangu wengi wanaweza kujitolea nafsi zao zote ili kujitumia kwa ajili Yako, lakini kimo changu ni kidogo sana. Nafikiria riziki yangu na mustakabali wangu, na pia iwapo nitaweza kuvumilia taabu ya mwili. Siwezi kuyaacha mambo hayo. Kweli nina deni Lako. Wanawezaje kuwa na kimo kama hicho? Usuli wa familia zetu ni sawa, lakini wanaweza kujitumia kwa ajili Yako wakati wote—mbona siwezi? Nakosa ukweli mwingi sana. Daima nafikiri juu ya matatizo ya mwili; imani yangu ni ndogo sana. Ee Mungu, naomba Unipe nuru na mwangaza, Ukiniruhusu kuwa na imani ya kweli Kwako na kujitumia kikamili kwa ajili Yako punde kabisa.” Huku ni kuzungumza kutoka moyoni. Ikiwa una aina hii ya mawasiliano ya dhati na Mungu kila siku, Ataona kwamba wewe ni mwaminifu, kwamba humfanyii vitu kwa namna isiyo ya dhati tu, kumpa maneno matamu Yeye au kumuunga mkono kwa maneno matupu tu. Kisha Roho Mtakatifu atafanya kazi Yake. Huu ndio mwanzo wa kuanzisha uhusiano ufaao na Mungu. Sisi ni viumbe walioumbwa, na Yeye ni Muumba. Sisi viumbe tulioumbwa tunapaswa kuwa na nini mbele ya Muumba wetu? Utiifu, ridhaa, imani na ibada ya kweli. Lazima tutoe mioyo yetu kwa Mungu kikamilifu; lazima tumwache aongoze, kutawala na kupanga. Kwa kuomba na kutafuta kwa njia hii, uhusiano wetu na Mungu utakuwa wa kufaa.

kutoka katika “Mahubiri na Ushirika Kuhusu Neno la Mungu ‘Ni Muhimu Sana Kuanzisha Uhusiano wa Kufaa na Mungu’ (I)” katika Mahubiri na Ushirika Kuhusu

Kuingia Katika Maisha XIV

Kuna kanuni kadhaa za kuanzisha uhusiano wa kufaa na Mungu. Ya kwanza ni kwamba lazima uamini katika uweza na hekima Yake, na lazima uamini kwamba maneno yote ya Mungu yatatimizwa. Huu ndio msingi. Ikiwa huamini kwamba maneno ya Mungu hakika yatatimizwa au kuamini katika uweza wa Mungu, basi huna imani ya kweli. Pili, lazima utoe moyo wako kwa Mungu na kumwacha Mungu kuamua katika mambo yote. Tatu, lazima ukubali uchunguzi wa Mungu, na hili ni muhimu. Usipokubali uchunguzi wa Mungu wa maombi na ushirika wako, matendo yako na maneno yako, utawezaje kuwa na ushirika wa kweli na Mungu? Utaweza kumwambia kile kilicho moyoni mwako? Unapozungumza, unaomba tu kwa ajili yako; lina nia mbaya, na limejaa maneno matupu, majisifu na uongo. Usipokubali uchunguzi wa Mungu, utawezaje kutambua mambo hayo? Punde utakapokubali uchunguzi wa Mungu, wakati umesema kitu kibaya, kuzungumza maneno matupu, au kutoa viapo vya kawaida, utatambua mara moja, “Je, sijaribu kumdanganya Mungu? Mbona hili linahisi kama kumdanganya Mungu?” Huku ni kukubali uchunguzi wa Mungu, na hii ndiyo maana ni muhimu sana. Nne, lazima ujifunze kutafuta ukweli katika mambo yote. Usitegemee falsafa ya Shetani; usitegemeze vitu kwa iwapo utafaidika au la. Lazima utafute ukweli na kutenda kulingana na ukweli. Bila kujali faida au hasara yoyote ya binafsi, lazima utende ukweli na kusema ukweli, na pia kuwa mtu mwaminifu. Kupitia hasara ni aina ya baraka; utabarikiwa zaidi na Mungu unapopitia hasara. Ibrahimu alipitia hasara nyingi, na daima aliafikiana katika kuingiliana kwake na wengine. Hata watumishi wake walilalamika, “Kwa nini wewe ni dhaifu sana? Acha tupigane nao!” Ibrahimu alikuwa akifikiri nini wakati huo? “Hatupigani nao. Kila kitu kiko mikononi mwa Mungu, na ni sawa kupitia hasara kiasi.” Kama matokeo, Mungu alimbariki Ibrahimu hata zaidi. Ikiwa faida zako binafsi zimetiwa hatarini kwa sababu ya kutenda kwako ukweli na humlaumu Mungu, basi Mungu atakubariki. Tano, lazima ujifunze kutii ukweli katika mambo yote; hili pia ni muhimu. Bila kujali ni nani anayesema kitu kinachokubaliana na ukweli, bila kujali iwapo ana uhusiano mzuri na sisi au la, na bila kujali jinsi tunavyohisi kumhusu, alimradi kile anachosema kinakubaliana na ukweli, tunapaswa kukitii na kukikubali. Hili linaonyesha nini? Kuwa na moyo wa uchaji kwa Mungu. Ikiwa mtu anaweza hata kumtii mtoto wa miaka tatu ambaye maneno yake yanakubaliana na ukweli, je, mtu huyu bado ana majivuno yoyote? Bado yeye ni mtu mwenye majivuno? Tabia yake imebadilishwa. … Sita, kuwa mwaminifu kwa Mungu katika kutimiza wajibu wako. Huwezi kamwe kusahau kutimiza wajibu wako kama kiumbe aliyeumbwa—usipofanya hivyo, hutawahi kamwe kumridhisha Mungu. Yeyote asiyetimiza wajibu wake ni takataka na ni wa Shetani. Kama unaweza kutimiza wajibu wako mbele ya Mungu basi wewe ni mmoja wa watu wa Mungu—hii ndiyo alama. Ukitimiza wajibu wako vizuri, wewe ni kumbe ambaye amefikia kiwango kilichowekwa; ukikosa kutimiza wajibu wako, basi hujafikia kiwango kilichowekwa na hutapata idhini ya Mungu. Kwa hiyo, ikiwa unaweza kuwa mwaminifu kwa Mungu katika kutimiza wajibu wako na kisha uwasiliane na Mungu, Atakosa kukubariki? Atakosa kuwa nawe? Saba, simama upande wa Mungu katika mambo yote; kuwa wa moyo na akili moja na Mungu. Wazazi wako wakisema chochote kisichokubaliana na ukweli, kinamchopinga na kumwasi Mungu, basi unapaswa kuweza kusimama na Mungu na kubishana nao, kuwakana, na kukataa kukubali kile wanachosema. Je, huku si kuwa na ushuhuda? Je, hili linaweza kumwaibisha Shetani? (Ndiyo, linaweza.) … Ikiwa watu wanaweza kutii kanuni hizi saba, wanaweza kupata idhini ya Mungu, na kisha uhusiano wao na Mungu utakuwa wa kufaa kabisa. Hizi kanuni saba ni muhimu sana!

kutoka katika “Mahubiri na Ushirika Kuhusu Neno la Mungu ‘Ni Muhimu Sana Kuanzisha Uhusiano wa Kufaa na Mungu’ (IV)” katika Mahubiri na Ushirika Kuhusu

Kuingia Katika Maisha XIV

Chanzo: Kanisa la Mwenyezi Mungu 

Views: 73 | Added by: flickrpinquorettfb | Tags: Roho Mtakatifu, neno la Mungu | Rating: 0.0/0
Total comments: 0
avatar