11:55 AM
Utendaji (3)

Lazima muwe na uwezo wa kuishi kwa kujitegemea, kuweza kula na kunywa maneno ya Mungu ninyi wenyewe, kupitia maneno ya Mungu ninyi wenyewe, na kuishi maisha ya kiroho ya kawaida bila uongozi wa wengine; lazima muweze kuyategemea maneno ya Mungu ya leo ili kuishi, kuingia katika uzoefu wa kweli, na kuona kwa hakika. Ni wakati huo tu ndipo mtaweza kusimama imara. Leo, watu wengi hawaelewi kikamilifu majonzi na majaribio ya siku za usoni. Katika siku za usoni, watu wengine watapitia majonzi, na wengine watapitia adhabu. Adhabu hii itakuwa kali zaidi; itakuwa ni kuwasili kwa ukweli. Leo, yote unayopitia, kufanya, na kuonyesha yanaweka msingi wa majaribio ya siku za usoni, na kwa kiwango cha chini mno, lazima uweze kuishi kwa kujitegemea. Leo, hali inayohusu wengi kanisani ni kama ifuatayo kwa jumla: Ikiwa kuna wafanyakazi wa kufanya kazi ya kanisa, wao wana furaha, na ikiwa hawapo, wao hawana furaha; na wao hawatilii maanani kazi ya kanisa, wala kula na kunywa kwao wenyewe, na hawana hata mzigo kidogo sana—wao ni kama ndege wa Hanhao.[a]Kusema kweli, ndani ya watu wengi kazi ambayo Nimefanya ni kazi ya ushindi tu, kwani wengi hawastahili kimsingi kufanywa wakamilifu. Ni sehemu ndogo tu ya watu ndio wanaweza kufanywa wakamilifu. Ikiwa, baada ya kuyasikia maneno haya, unaamini kwamba kazi inayofanywa na Mungu ni kwa ajili tu ya kuwashinda watu, na hivyo unafuata tu kwa uzembe, mwelekeo wa aina hiyo ungewezaje kukubalika? Ikiwa kweli unamilikiwa na dhamiri, basi lazima uwe na mzigo, na hisia ya kuwajibika. Lazima useme: Sijali kama nitashindwa au kufanywa mkamilifu, lakini lazima niwe na hatua hii ya ushuhuda kwa kufaa. Kama kiumbe wa Mungu, mtu anaweza kushindwa kabisa na Mungu, na hatimaye, aweze kumridhisha Mungu, kulipa upendo wa Mungu kwa upendo ulio ndani ya moyo wake na kwa kujitolea mwenyewe kabisa kwa Mungu. Huu ni jukumu wa mwanadamu, ni wajibu unaopaswa kutekelezwa na mwanadamu, na mzigo unaopaswa kubebwa na mwanadamu, na mwanadamu lazima atimize agizo hili. Ni wakati huo tu ndipo wanaamini katika Mungu kwa hakika. Leo, kile unachofanya kanisani ni timizo la wajibu wako? Hili linategemea na kama una mzigo, na kutegemea maarifa yako mwenyewe. Katika kuipitia kazi hii, ikiwa mwanadamu anashindwa na ana maarifa ya kweli, basi utaweza kutii bila kujali matazamio au majaliwa yako mwenyewe. Kwa njia hii, kazi kuu ya Mungu itafanywa yote kabisa, kwani watu hawa hawawezi kufanya lolote zaidi ya hili, na hawawezi kutimiza mahitaji yoyote ya juu zaidi. Ilhali katika siku za usoni, watu wengine watafanywa wakamilifu. Uhodari wao utakuwa mzuri zaidi, ndani ya roho zao watakuwa na maarifa ya kina zaidi, maisha yao yatakua.... Ilhali wengine hawawezi kabisa kulitimiza hili, na hivyo hawawezi kuokoka. Kuna sababu ya Mimi kusema kwamba hawawezi kuokoka. Katika siku za usoni, wengine watashindwa, wengine wataondoshwa, wengine watafanywa wakamilifu, na wengine watatumiwa—na kwa hiyo wengine watapitia majonzi, wengine watapitia adhabu (majanga ya asilia pamoja na misiba inayosababishwa na mwanadamu), wengine wataondoshwa, na wengine watasalia. Katika hili, kila mmoja ataainishwa kulingana na aina, na kila kikundi kikiwakilisha aina ya mtu. Sio watu wote wataondoshwa, wala watu wote kufanywa wakamilifu. Hili ni kwa sababu uhodari wa watu wa China ni duni sana, na kuna idadi ndogo sana pekee miongoni mwao walio na aina ya kujitambua ambayo Paulo alikuwa nayo. Miongoni mwa watu hawa, wachache wana azimio la kumpenda Mungu sawa na la Petro, au aina ya imani kama ya Ayubu. Wachache sana kati yao wana kiwango sawa cha heshima kwa Yehova, au kiwango sawa cha uaminifu katika kumhudumia Yehova kama Daudi. Mnasikitisha jinsi gani!

Leo, mazungumzo juu ya kufanywa mkamilifu ni hali moja tu. Haijalishi kinachofanyika, lazima muwe na hatua hii ya ushuhuda kwa kufaa. Kama mngeulizwa mumhudumie Mungu katika hekalu, mngefanyaje hivyo? Kama hungekuwa kuhani, na hungekuwa na cheo cha wana wazaliwa wa kwanza au wana wa Mungu, bado ungeweza kuwa mwaminifu? Bado ungeweza kufanya yote unayoweza ili kuueneza ufalme? Bado ungeweza kufanya kazi ya agizo la Mungu kwa kufaa? Haijalishi vile maisha yako yamekua, kazi ya leo itakusababisha uridhishwe kabisa ndani yako, na uweke kando dhana zako zote. Kama una kinachohitajika kuyafuatilia maisha au la, kwa jumla, kazi ya Mungu itakufanya uridhike kabisa. Watu wengine husema: Naamini katika Mungu, lakini sielewi ni nini maana ya kuyafuatilia maisha. Na wengine husema: Mimi nimetatanishwa katika imani yangu kwa Mungu. Najua kwamba siwezi kufanywa mkamilifu, kwa hivyo niko tayari kuadibiwa. Hata watu kama hawa, ambao wako tayari kuadibiwa au kuangamizwa, lazima washurutishwe kukubali kwamba kazi ya leo inafanywa na Mungu. Watu wengine pia husema: Siombi kufanywa mkamilifu, lakini, leo, niko radhi kukubali mafundisho yote ya Mungu, na niko radhi kuishi kwa kudhihirisha ubinadamu wa kawaida, kuendeleza uhodari wangu, na kutii mipango yote ya Mungu..... Katika hili, wao pia wameshindwa na kuwa na ushuhuda, ambalo linathibitisha kwamba kuna maarifa fulani ndani ya watu hawa. Hatua hii ya kazi imetekelezwa haraka kabisa, na katika siku za usoni, itatekelezwa hata haraka zaidi ng'ambo. Leo, watu walio ng'ambo hawawezi kungoja, wote wanakimbilia China—na kwa hiyo ikiwa hamwezi kufanywa wakamilifu, mtakuwa mnawashikilia watu walio ng'ambo. Wakati huo, haijalishi vile mlivyo, wakati utakapofika kazi Yangu itahitimishwa na kutimizwa! Sijali kuhusu vile ambavyo mmeingia vizuri au mlivyo ninyi; kazi Yangu yote haiwezi kushikiliwa nanyi. Nafanya kazi ya wanadamu wote, na hakuna haja ya Mimi kutumia muda wowote zaidi kwenu! Ninyi ni wasio na motisha kabisa, wanaokosa kujitambua kabisa! Hamstahili kufanywa wakamilifu—mna uwezo mdogo sana! Katika siku za usoni, hata watu wakiendelea kuwa wazembe na hobelahobela sana, na kubaki wasioweza kuendeleza uhodari wao, hili halitazuia kazi ya ulimwengu mzima. Wakati ukifika wa kazi ya Mungu kumalizika, itamalizika, na wakati ukifika wa watu kuondoshwa, wataondoshwa. Bila shaka, wale wanaopaswa kufanywa wakamilifu, na wanastahili kufanywa wakamilifu, pia watafanywa wakamilifu—lakini ikiwa hamna tumaini kabisa, basi kazi ya Mungu haitawangoja ninyi! Hatimaye, ukishindwa, hili pia linaweza kufikiriwa kama kuwa na ushuhuda; kuna mipaka kwa kile ambacho Mungu anakutaka ufanye. Hata kama kimo ambacho mwanadamu anaweza kutimiza ni cha juu kiasi gani, urefu wa ushuhuda wake unatakiwa kuwa hivyo. Sio kama anavyofikiria mwanadamu kwamba ushuhuda kama huo utafikia mipaka ya juu zaidi na kwamba utakuwa mkubwa sana—hakuna vile hili linaweza kutimizwa ndani ya ninyi watu wa China. Nimeshirikiana nanyi kwa wakati huu wote, na ninyi wenyewe mmeona hili. Nimewaambia msipinge, msiwe waasi, msifanye mambo ya aibu bila Mimi kufahamu. Nimewaambia maneno haya bayana mara nyingi, lakini hata hilo halitoshi—mara tu Ninapogeuka wao hubadilika, na wengine hunipinga Mimi kisirisiri, bila majuto yoyote. Unadhani sijui lolote hili? Unadhani unaweza kunisababishia Mimi matatizo na hakuna kitakachotokea? Unadhani sijui unapojaribu kubomoa kazi Yangu bila Mimi kufahamu? Unadhani kwamba hila zako ndogo zinaweza kushikilia nafasi ya hulka yako? Wewe kila mara unaonekana kuwa mtiifu lakini wewe ni mdanganyifu kisirisiri, unaficha mawazo mabaya ndani ya moyo wako, na hata kifo si adhabu ya kutosha kwa watu kama wewe. Unadhani kwamba kazi kidogo inayofanywa na Roho Mtakatifu ndani yako inaweza kuchukua nafasi ya uchaji wako Kwangu? Unafikiri ulipata nuru kupitia kwa kuiita Mbinguni? Wewe huna aibu! Wewe huna thamani kabisa! Unafikiria kwamba "matendo yako mema" yamegusa Mbinguni, ambayo imefanya jambo la pekee na imekupa vipawa vya asilia vilivyokufanya uwe na lugha ya kushawishi, iliyokukubalia kuwadanganya wengine, na kunidanganya Mimi? Wewe ni mkosa urazini kweli! Je, wajua mahali ambapo nuru yako inatoka? Je, hujui ulikula chakula cha nani ulipokuwa unakua? Wewe ni wa kupita kiasi kweli! Wengine miongoni mwenu hawajabadilika hata baada ya miaka minne au mitano ya kushughulikiwa; mnaelewa kuhusu mambo haya, mnapaswa kuelewa asili yenu—na kwa hiyo msipinge wakati ambapo, siku moja, mtatelekezwa. Wengine, ambao hudanganya wale walio juu na chini yao katika huduma yao, wamepitia ushughulikiaji mwingi sana; wengine, kwa sababu ni wenye tamaa ya pesa, wamepitia ushughulikiaji mwingi sana; wengine, kwa sababu hawaweki mipaka iliyo wazi baina ya wanaume na wanawake, wamepitia ushughulikiaji mwingi sana, wengine kwa sababu ni wavivu, wanaofikiria tu juu ya mwili, na hawatendi haki wanapofika kanisani, wamepitia ushughulikiaji mwingi sana, wengine kwa sababu hukosa kuwa na ushuhuda popote waendapo, na hutenda dhambi na kukosa adabu kwa makusudi, wamekumbushwa mara nyingi; wengine huzungumza kuhusu maneno na mafundisho ya dini wanapofika kanisani, wanajiona wao ni wa cheo cha juu kuliko wengine wote, na hawana uhalisi hata kidogo sana, huku ndugu wakila njama miongoni mwao wenyewe, wakishindana wenyewe kwa wenyewe—wamefichuliwa mara kwa mara kwa sababu ya hili. Nimezungumza maneno haya kwenu mara nyingi sana, na leo, Sitazungumza tena kuhusu hili—fanyeni mtakalo! Fanyeni uamuzi wenu wenyewe! Watu wengi hawajapitia tu ushughulikiaji huu kwa mwaka mmoja au miwili tu, kwa wengine imekuwa miaka mitatu au minne, na wengine wamepitia hili kwa zaidi ya mwongo mmoja, wakiwa wamepitia ushughulikiaji walipogeuka kuwa waumini, lakini kufikia sasa kumekuwa na mabadiliko madogo ndani yao. Unasema nini, wewe sio kama nguruwe? Je, huku ni kukuonea wewe? Msifikiri kwamba kazi ya Mungu haitamalizika ikiwa hamwezi kufikia kiwango fulani. Je, Mungu bado atawangoja ikiwa hamwezi kutimiza matakwa Yake? Nawaambia waziwazi—sivyo hivyo! Usiwe na mtazamo kama huo wa kutia matumaini kuhusu mambo! Kuna muda maalum kwa kazi ya leo hii, Mungu hachezi tu na wewe! Hapo awali, ilipofikia kupitia majaribio ya watendaji huduma, watu walifikiri kwamba kwa wao kusimama imara katika ushuhuda wao kwa Mungu, walitakiwa kushindwa kwa kiwango fulani—walitakiwa kuwa watendaji huduma kwa hiari na kwa furaha, na walitakiwa kumsifu Mungu kila siku, na wasiwe wazembe au wa harara hata kidogo. Walifikiri kwamba ni wakati huo tu ndipo wangekuwa watendaji huduma kweli, lakini hali ni hiyo kwa kweli? Wakati huo, kulikuwa na kila aina ya maonyesho ndani ya watu. Wengine walikimbia, wengine walimpinga Mungu, wengine walifuja pesa za kanisa, na ndugu walikula njama dhidi yao wenyewe, wakilaani na kutukanana wenyewe kwa wenyewe. Ulikuwa ukombozi mkubwa kweli, lakini kulikuwa na kitu kimoja kizuri kulihusu: Hakuna aliyerudi nyuma. Hiki ni kitu bora zaidi kinachoweza kusemwa kulihusu. Walikuwa na ushuhuda mbele ya Shetani kwa sababu ya hili, na baadaye walipata utambulisho wa watu wa Mungu na wakafaulu hata kufikia leo. Kazi ya Mungu haitekelezwi unavyofikiria. Muda ukiisha, kazi hiyo itaisha, haijalishi vile ulivyo. Watu wengine huenda wakasema: Kwa kutenda hivi Huwaokoi watu, au kuwapenda—Wewe si Mungu mwenye haki. Nakwambia waziwazi: Kiini cha kazi Yangu leo ni kukushinda wewe na kukufanya uwe na ushuhuda. Kukuokoa wewe ni kiongezo tu; kama unaweza kuokolewa au la hutegemea ufuatiliaji wako mwenyewe, na hakuhusiani na Mimi. Ilhali lazima Nikushinde wewe; usijaribu kila mara kunidhibiti Mimi—leo Ninakufinyanga, sio vinginevyo!

Leo, kile ambacho mmepata kuelewa ni cha juu zaidi kuliko mtu yeyote kote katika historia ambaye hakufanywa mkamilifu. Iwe ni ufahamu wenu wa majaribio au imani katika Mungu, yote ni ya juu zaidi kuliko ya muumini yeyote katika Mungu. Mambo mnayoyafahamu ni yale mnayokuja kujua kabla ya ninyi kupitia majaribio ya mazingira, lakini kimo chenu halisi hakipatani nayo. Kile mnachojua ni cha juu zaidi kuliko kile mnachotia katika vitendo. Ingawa mnasema kwamba watu wanaoamini katika Mungu wanapaswa kumpenda Mungu, na hawapaswi kupania baraka bali kuyaridhisha tu mapenzi ya Mungu, kinachoonekana katika maisha yenu ni tofauti kabisa na hili, na kimewekwa mawaa kabisa. Watu wengi huamini katika Mungu kwa ajili ya amani na manufaa mengine. Isipokuwa kwa manufaa yako, wewe huamini katika Mungu, na ikiwa huwezi kupokea neema za Mungu, wewe huanza kununa. Hiki kingekuwaje kimo chako halisi? Inapofikia matukio ya familia yasiyoepukika (watoto kuwa wagonjwa, mume kwenda hospitalini, mazao mabaya ya mimea, kuteswa kwa watu wa familia, na kadhalika), huwezi hata kufaulu katika mambo haya ambayo hufanyika mara kwa mara katika maisha ya kila siku. Wakati ambapo mambo hayo hufanyika, wewe huingia katika hofu kubwa, hujui la kufanya—na wakati mwingi, wewe hulalamika kuhusu Mungu. Wewe hulalamika kwamba maneno ya Mungu yalikudanganya, kwamba kazi ya Mungu imekuvuruga wewe. Je, hamna mawazo kama haya? Unadhani mambo kama haya hufanyika miongoni mwenu mara chache tu? Mnatumia kila siku kuishi katikati ya matukio kama haya. Hamfikirii hata kidogo sana kuhusu mafanikio ya imani yenu katika Mungu, na namna ya kuyaridhisha mapenzi ya Mungu. Kimo chenu halisi ni kidogo sana, hata kidogo zaidi kuliko cha kifaranga mdogo. Wakati ambapo biashara ya waume zenu hupoteza pesa ninyi hulalamika kuhusu Mungu, wakati ambapo ninyi hujikuta katika mazingira yasiyo na ulinzi wa Mungu ninyi bado hulalamika kuhusu Mungu, ninyi hulalamika hata wakati ambapo mmoja wa vifaranga wenu hufa au ng'ombe mzee ndani ya zizi anapougua, ninyi hulalamika kama ni wakati wa wana wenu kuanzisha familia lakini familia yenu haina pesa za kutosha, na wakati ambapo wafanyakazi wa kanisa hula milo kadhaa nyumbani kwako lakini kanisa halikulipi au hakuna anayekutumia mboga zozote, wewe hulalamika pia. Tumbo lako limeshindiliwa pomoni na malalamiko, na wakati mwingine wewe huendi katika mikutano au kula na kunywa maneno ya Mungu kwa sababu ya hili, wewe huelekea kuwa mbaya kwa muda mrefu sana. Hakuna chochote kinachokufanyikia leo hii kilicho na uhusiano wowote na matazamio au majaliwa yako; mambo haya yangefanyika pia ikiwa hungeamini katika Mungu, ilhali leo hii unampitishia Mungu wajibu wa haya mambo, na kusisitiza kusema kwamba Mungu amekuondosha wewe. Na kuhusu imani yako katika Mungu, je, umeyatoa maisha yako kwa kweli? Mngepitia majaribio sawa na yale ya Ayubu, hakuna hata mmoja miongoni mwenu anayemfuata Mungu leo hii angeweza kusimama imara, nyote mngeanguka chini. Na kunayo, kawaida kabisa, tofauti kubwa kati ya ninyi na Petro. Leo, kama nusu ya mali yenu ingetwaliwa mngethubutu kukana kuwepo kwa Mungu; kama mtoto wenu wa kiume au wa kike angechukuliwa kutoka kwenu, mngekimbia barabarani mkilalamika vikali; kama maisha yako yangegonga mwamba, ungejaribu kuanza kujadiliana mada hiyo na Mungu, ukiuliza kwa nini Nilisema maneno mengi sana hapo mwanzo kukutisha wewe. Hakuna kitu chochote ambacho hamngethubutu kufanya katika nyakati kama hizi. Hili linaonyesha kwamba hamjaona kwa kweli, na hamna kimo cha kweli. Hivyo, majaribio yaliyo ndani yenu ni makubwa mno, kwani ninyi huelewa mengi sana, lakini mnachojua kweli sio hata sehemu moja kwa elfu ya kile mnachofahamu. Msikomee kwa ufahamu na maarifa pekee; mngeona vyema kiasi gani mnachoweza kutia katika vitendo kwa kweli, kiasi gani cha jasho la kazi yenu ngumu imegeuzwa kuwa kupata nuru na mwangaza wa Roho Mtakatifu, na katika matendo mangapi yenu mmetambua azimio lenu wenyewe. Unapaswa kuchukua kimo chako na kutenda kwa dhati. Katika imani yako kwa Mungu, hupaswi tu kujaribu kufanya mambo kwa namna isiyo ya dhati kwa ajili ya yeyote—kama unaweza kupata au la hutegemea ufuatiliaji wako mwenyewe.

Tanbihi:

a. Hadithi ya ndege wa Hanhao inafanana sana na hekaya ya Aesop ya mchwa na panzi. Ndege wa Hanhao anapendelea kulala badala ya kujenga kiota wakati hali ya hewa ni ya vuguvugu—licha ya maonyo ya tena na tena kutoka kwa jirani yake, ndege wa jamii ya kunguru. Wakati ambapo majira ya baridi kali hufika, ndege huyo huona baridi sana hadi kufa.

kutoka katika Neno Laonekana katika Mwili

Chanzo: Kanisa la Mwenyezi Mungu 

Views: 60 | Added by: flickrpinquorettfb | Tags: Matamshi ya Kristo, upendo wa Mungu | Rating: 0.0/0
Total comments: 0
avatar